Wednesday , 23rd Jan , 2019

Baada ya Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Duniani FIFA kumfungia maisha aliyekuwa Makamu wa Rais, Michael Richard Wambura kujihusisha na masuala yoyote ya mpira wa miguu, Shirikisho la Soka nchini TFF limetoa onyo zito.

Michael Wambura

Onyo hilo lililotolewa kuanzia jana Januari 22, limetumwa na Kamati hiyo ya Nidhamu chini ya Mwenyekiti wake, Anin Yeboah. Ikiunga mkono hukumu ya Kamati ya Rufani na Maadili ya TFF iliyotolewa April 6, 2018.

Katika taarifa yake kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, TFF imetoa onyo kali kwa wadau wa soka juu ya kufuata sheria na maadili ya shirikisho hilo.

"TFF tayari imeshamkabidhi Wambura uamuzi huo, na inawakumbusha wana familia ya mpira wa miguu kuzingatia maadili na nidhamu kwa kufuata taratibu zake kwa mujibu wa Katiba za TFF, CAF na FIFA", imesema taarifa hiyo.

Michael Wambura alichaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka nchini TFF katika uchaguzi mkuu wa mwezi Julai mwaka 2017, kabla ya kufungiwa na shirikisho hilo mwaka uliopita kwa tuhuma za matumizi mabaya ya fedha.

Alikata rufaa Mahakamani, ambapo Mahakama iliamuru kurejeshwa katika nafasi yake mwishoni mwa mwaka uliopita lakini TFF ilikata rufaa FIFA.