Monday , 8th Dec , 2014

Shirikisho la Ngumi nchini BFT limesema baada ya kumaliza mashindano ya Ngumi ya wazi ya Taifa yaliyoanza Desemba tatu mpaka sita Uwanja wa ndani wa Taifa jijini Dar es salaam,limeanza zoezi la kuunda timu mpya ya Taifa itakayokaa kambi ya muda mrefu

Akizungumza na East Africa Radio,Makamu wa Rais wa BFT,Lukelo Wililo amesema wameshaiagiza kamati ya Ufundi ya BFT pamoja na Makocha wa timu zilizopo mikoani kuchagua mabondia wenye vigezo kwa ajili ya kujiunga na kambi hiyo inayotarajiwa kuanza mapema mwakani.

Wililo amesema baada ya kupatikana kwa mabondia hao,Kamati kuu ya Utendaji ya BFT inaangalia uwezo wa Mabondoa hao kama wanakidhi vigezo kwa ajili ya kuuanda kambi ya Timu ya Taifa itakayoweza kushiriki mashindano mbalimbali makubwa ya ndani na nje ya nchi.

Wililo amesema katika mashindano ya ngumi taifa,wameona vipaji vipya vya vijana kutoka mikoa mbalimbali Tanzania ambapo wanaamini vijana hao wanauwezo wa kufanya vizuri kwa ajili ya kurudisha hadhi ya mchezo wa ngumi hapa nchini.