
Mbwana Samatta na ligi ya Ubelgiji
Ligi hiyo maarufu kama 'Jupiter Pro League' ambayo anachezea mshambuliaji na nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta ndiyo inatumia mfumo huo ili kumpata bingwa wa ligi na mwakilishi wa michuano ya Klabu Bingwa Barani Ulaya.
Klabu ya KRC Genk anayochezea Samatta inaongoza ligi mpaka sasa kwa pointi 51, tofauti ya poiti 7 dhidi ya Club Brugge inayoshika nafasi ya pili, hivyo kumekuwa na maswali mengi kwa mashabiki wa soka hapa nchini juu ya uwezekano wa timu hiyo kuwa bingwa mwishoni mwa msimu huu, wengine wakisema kuwa hatoweza kuwa bingwa kutokana na hatua nyingine inayofuata baada ya ligi kumalizika.
Zifuatazo ni baadhi ya dondoo zitakazokupa ufahamu juu ya namna bingwa wa ligi hiyo anavyopatikana.
Msimu wa 2009/10 mfumo wa ligi hiyo ulifanyiwa marekebisho ambapo mfumo wa kucheza michezo ya mchujo 'Playoffs' baada ya ligi kumalizika ulianzishwa.
Mfumo huo unahusisha timu 6 zilizo juu ya msimamo wa ligi mwishoni mwa msimu, ambapo kila timu hucheza mechi mbili dhidi ya mpinzani wake na kupimwa kwa pointi. Timu itakayokuwa juu ya msimamo itakuwa bingwa wa ligi hiyo pamoja na kupata nafasi ya kushiriki michuano ya Klabu Bingwa Ulaya sambamba na mshindi wa pili.
Bingwa wa kombe la Ubelgiji (Belgian Cup) pamoja na timu iliyo nafasi ya tatu baada ya michezo ya 'Playoffs', zitafuzu kucheza michuano ya Europa League zikianzia hatua ya kufuzu.