Tuesday , 13th Nov , 2018

Klabu ya soka ya KMC inayoshiriki ligi kuu soka Tanzania bara msimu huu, imeanza kufanya usajili kabla ya dirisha dogo kufunguliwa rasmi kwa kunasa sahihi ya mshambuliaji Elias Maguli.

Mchezaji Elias Maguli (kulia) akitambulishwa leo.

KMC imemtangaza Maguli leo kwenye mkutano na wanahabari katika ukumbi wa manispaa ya Kinondoni, mtaa wa Magomeni. Maguli ambaye alikuwa akiichezea AS Kigali ya Rwanda amesaini mkatabwa wa mwaka mmoja kuichezea timu hiyo ya vijana wa Kinondoni.

Afisa Habari wa KMC Anwar Binde amesema Maguli ni chaguo na pendekezo la mwalimu Ettiene Ndayiragije katika kuendelea kuimalisha kikosi chake kwaajili ya kuongeza ushindani zaidi.

Aidha Binde amebainisha kuwa bado wanaendelea na mazungumzo na baadhi ya nyota na muda ukifika na dirisha kufunguliwa watawatambulisha. KMC imefuata nyayo za Azam FC ambayo nayo imemsajili mshambuliaji Obrey Chirwa hivi karibuni kabla ya dirisha dogo kufunguliwa.

Mbali na KMC na AS Kigali Maguri amewahi kuchezea Dhofar SC ya Oman, Ruvu Shooting ya Pwani, Stand United ya Shinyanga na Simba SC ya Dar es Salaam.