Tuesday , 5th Feb , 2019

Tofauti ya pointi kati ya kinara wa ligi Liverpool na anayeshika nafasi ya pili Manchester City inaendelea kushuka siku hadi siku na kuhatarisha mbio zake za ubingwa wa kwanza baada ya miaka 29 kupita.

Javier Hernandez 'Chicharito' wa West Ham akiwa katikati ya wachezaji wa Liverpool, usiku wa jana.

Kabla ya Januari 3, 2019, Liverpool ilikuwa ikiongoza ligi kwa tofauti ya pointi 7 na Manchester City iliyokuwa nafasi ya pili, mpaka sasa tofauti ya pointi kati ya timu hizo ni tatu pekee. Katika kipindi cha mwezi mmoja, Liverpool imefungwa mechi moja, na kutoka sare mechi mbili.

Matokeo hayo mabovu yamechangiwa na sababu nyingi ambazo wengi wanaamini, ikiwemo majeruhi ilio nao, ambapo jumla ya wachezaji 5 muhimu wanakosekana uwanjani. Lakini sababu nyingine ni kutokuwa na kikosi kipana chenye uzoefu ukilinganisha na kikosi kama cha Manchester City ambacho akitoka mchezaji mmoja nje, nafasi yake inazibwa na mchezaji mwenye kiwango sawa naye au zaidi.

Kwa mashabiki wa Liverpool watakumbuka vizuri namna Chelsea ilivyowaharibia shughuli ya ubingwa msimu wa 2013/14 baada ya Steven Gerrard kuteleza eneo la hatari na mshambuliaji Demba Ba kufunga kirahisi karibia mwishoni mwa msimu, kitu kama hicho ndicho kinachoendelea hivi sasa ndani ya Liverpool, na hatari yake ni kwamba wao wanavyozidi kudondosha pointi, Man City inashinda tena kwa vipigo vya kuudhi.

Cha kufurahisha hapa ni kwamba msimu huu pia Liverpool itakutana na Chelsea katika mchezo wa 34 wa ligi, kama ilivyokuwa msimu wa 2013/14 ambao ndoto za ubingwa wao ziliishia mikononi mwa Manchester City, hatujui hali itakuwaje huko hasa ukizingatia Chelsea ipo katika mstari wa hatari, ikipigania nafasi ya kushiriki michuano ya Klabu Bingwa Ulaya msimu uliopita.

Liverpool inahitaji kucheza kwa malengo katika kila mchezo, lazima watambue kuwa kila timu inayokutana nayo hivi sasa inataka kuwakamia kwasababu tuu wao wapo kileleni mwa ligi, inatakiwa kuchagua kipaumbele kati ya ubingwa wa EPL au Klabu Bingwa Barani Ulaya.