Tuesday , 23rd Jan , 2018

Msanii wa Bongo Fleva Madee, amefunguka kuhusu usajili uliofanywa na timu za Manchester United na Arsenal kwa kubadilishana wachezaji Alexis Sanchez na Henrick Mkhitaryan.

Madee anayetamba na ngoma ya 'Sema' aliyomshirikisha Nandy ni shabiki mkubwa wa klabu ya Arsenal na amesema ni mapema sana kujua kati ya timu hizo mbili ni nani kalamba dume.

''Ni mapema sana kukiri moja kwa moja kama Arsenal watakuwa wamefanikiwa kwenye huu usajili au Manchester United wamefanikiwa mpaka tusubiri tuone mechi mbili au tatu ndio tunaweza kujua timu gani imefanikiwa'', amesema Madee.

Aidha Madee ameongeza kuwa kwa kutumia uzoefu wa EPL, Sanchez ana nafasi kubwa ya kuonekana usajili mzuri kwa Manchester United, lakini hiyo pekee haitoshi kufanya mashabiki waamini kwani kuna wachezaji wengi walisajiliwa na wakashindwa kuonesha makali.

Madee ametolea mfano usajili ambao klabu ya Manchester United iliwahi kuufanya wa kumnunua Angel Di Maria kutoka Real Madrid lakini alishindwa kuwika kama ilivyodhaniwa Mwanzo.