Tuesday , 23rd Feb , 2016

Rais wa shirikisho la mpira wa miguu nchini TFF, Jamali Malinzi hii leo amegeuka mbogo kufuatia kuulizwa swali ambalo limemlenga yeye kuwa amehusika katika upangaji wa matokeo wa mechi za mwisho za kundi C ligi daraja la kwanza msimu uliomalizika.

Akizungumza mbele ya waandishi wa habari Malinzi amesema yeye ni mtu mzima na anaongoza taasisi kubwa hapa nchini anajua nini kinachoendelea kwa sasa akimaanisha kuna ajenda ya siri inaendeshwa dhidi yake.

Malinzi ameongeza kuwa kwa watu wanaoendesha ajenda hiyo waende wakaripoti kituo chochote cha polisi juu ya sakata hilo ili kama anahusika na upangaji wa matokeo achukuliwe hatua za kisheria licha ya kuonya kuwa kwa mwenendo huu watu hao wanaomhusisha yeye hawalipeleki popote soka la Tanzania.

Hii inatokana na taarifa za minong’ono zinazozungumzwa na baadhi ya wadau kua raisi huyo amekua akifanya mawasiliano na moja ya viongozi wa timu hizo wakati mechi inaendelea

Katika hatua nyingine Malinzi ametoa ufafanuzi kuwa jambo hilo ni kubwa na linatakiwa kufanyiwa uchunguzi wa kina hivyo kamati husika inataraji kusikiliza kesi hiyo siku ya tarehe 20 ya mwezi wa tatu mwaka huu.

Malinzi amesisitiza kuwa suala la upangaji wa matokeo ni janga ambalo wao kama TFF wanalipinga kila siku kama ilivyo kwa mataifa yaliyoendelea ambayo katika kanuni za mashindano zinaainisha adhabu kali kwa wanaokutwa na hatia.

Hata hivyo Malinzi ameongeza kuwa kanuni za mashindano hapa nchini hazina kipengele kinachotoa adhabu kama za kifungo cha maisha cha kutojihusisha na soka kwa wanaokutwa na hatia au kushushwa daraja kwa timu husika hali iliyowalazimu kulipeleka suala hilo katika kamati ya nidhamu.

Viashiria vya rushwa vilionekana katika mechi zilizokutanisha klabu za JKT Kanembwa na Geita Gold sambamba na Polisi Taboro dhidi ya JKT Oljoro ambazo zilifungana kwa bao 8-0 na nyingine 7-0.