Wednesday , 24th Jan , 2018

Kocha wa Paris Saint-Germain Unai Emery amesema nyota wa timu hiyo Mbrazil Neymar jr anapendwa na mashabiki wa timu hiyo tofauti na watu wanavyosema kuwa mashabiki wanamzomea.

''Neymar anaungwa mkono na mashabiki wote wa PSG na anapendwa sana kwasababu anafanya kazi kubwa uwanjani na kuinufaisha timu'', amesema Unai.

Siku za hivi karibuni Neymar amekuwa na wakati mgumu baada ya baadhi ya mashabiki wa timu hiyo kuanza kumzomea haswa baada ya kuamua kupiga mkwaju wa Penalti kwenye ushindi wa mabao 8-0 ambao PSG iliupata dhidi ya Dijon wiki iliyopita.

Mashabiki walimlalamikia Neyamr kuwa mkwaju huo alitakiwa kumwachia mshambuliaji Edinson Cavani ili apige kwasababu alikuwa nahitaji bao moja tu kuvunja rekodi ya Zlatan Ibrahimovic ya kuwa mfungaji bora wa muda wote wa klabu hiyo.

Tangu ajiunge na PSG akitokea Barcelona kwenye majira ya kiangazi Neymar amefanikiwa kufunga mabao 24 katika mechi 23 alizoicheza timu hiyo katika mashindano yote.