Thursday , 18th Feb , 2016

Kampuni ya vifaa vya michezo, Nike imeondoa udhamini wake kwa bondia na mwanasiasa wa Ufililipino Manny Pacquiao juu ya matamshi yake ya kuwabagua wenye mahusiano ya kimapenzi ya jinsia moja.

Pacquiao, anayewania jimbo moja huko Ufilipino katika nafasi ya useneta, aliwaita watu wanaoshughulika na mapenzi ya jinsia moja kuwa "wabaya zaidi ya wanyama", ingawa baadaye aliomba radhi.

"Tunaona maneno ya Pacquiao ni ya chuki".Ilisema taarifa ya Nike.

"Nike inapinga vikali ubaguzi wa aina yoyote na ina historia ndefu ya kutetea na kusimamia haki za watu wenye kujishughulisha na mapenzi ya jinsia moja".

Nike iliongeza kwa kuandika: "Hatuna tena mahusiano na Manny Pacquiao."

Pacquiao alitoa maneno hayo ya kupinga ushoga na usagaji kwenye Televisheni na baaadaye akatetea msimamo wake wa kupinga jamii hiyo kwa kusema "Nimeeleza ukweli wa kilichoandikwa na Biblia".

Pacquiao, alipigana pambano la mwisho Mei mwaka uliopita na kudundwa na Mmarekani Floyd Mayweather, lakini hivi sasa anajiandaa kurejea ulingoni dhidi ya Timothy Bradley Jr huko Las Vegas April mwaka huu.