Monday , 12th Dec , 2016

Aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage, ameibuka na kuunga mkono mabadiliko ya katiba ya timu hiyo yaliyopitishwa na mkutano wake mkuu wa dharura siku ya jana Jumapili ya Desemba 11, 2016

Ismail Rage - Mwenyekiti wa zamani wa Simba

 

Rage ambaye ni miongoni mwa wanachama wenye heshima wa Simba, amesema anaungana na wengi walioamua kwa nia moja kufanya mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo, na kuwataka wanaopinga kuacha kusababisha vurugu na kwamba wanapaswa kukubali kwa kuwa ndiyo maamuzi ya wengi.

Pia ameushauri uongozi wa klabu hiyo kutafuta wataalamu wazuri ili kuiandika vizuri katiba hiyo, ili isikwame pindi itakapofika kwa Msajili huku akiwa na imani kuwa kila mwanachama ataelewa maana ya mabadiliko hayo na hakutakuwa na vurugu za aina yoyote.

Klabu ya Simba siku ya jana ilifanya mabadiliko ya Katiba yanayoruhusu mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo kupitia mkutano wake mkuu wa dharuara uliofanyika katika bwalo la maafisa wa polisi, Oysterbay, Dar es Salaam.