Sunday , 17th Jul , 2016

Mhispania Rodriguez ameanza kuleta sumu za tiktak kwenye kikosi cha Azam FC baada ya kuiongoza timu hiyo kwa mara ya kwanza kama kocha, ikipata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Ashanti FC ya daraja la kwanza.

Kiungo Mudathir Yahya alianza kuifungia Azam dakika ya 69 kwa shuti la kiufundi kufuatia pasi ya kiungo Frank Domayo, kabla ya Abdallah Masoud 'Cabaye' kufunga bao la pili dakika ya 81 kwa shuti zuri la umbali wa mita 30.

Rodriguez, aliyeanza kazi kama kocha mpya wa Azam hivi karibuni, akichukua nafasi ya Muingereza Stewart Hall, alipanga vikosi viwili tofauti kipindi cha kwanza akiwaanzisha Juan Jesus Gonzalez, Wazir Salum, Erasto Nyoni, Aggrey Morris, Himid Mao, Kipre Bolou, Jean Mugiraneza, Ramadhani Singano 'Messi', Ibrahima Fofana, Shaaban Idd na Salum Abubakar 'Sure Boy' ambao wote aliwatoa kipindi cha pili na kuingiza wengine.