Tuesday , 10th May , 2016

Kocha wa Timu ya Taifa ya Vijana ya Tanzania Serengeti Boys Bakari Shime amewataka watanzania wasisubiri ushindi ndio waanze kuipa sapoti timu bali wanatakiwa kuanza nayo mwanzo ili kuweza kuwa nao pamoja mpaka mwisho.

Shime amesema, kesho anaondoka na kikosi akiwa kimya lakini akiamini anarudi na ushindi lakini Watanzania wasitegemee matokeo mazuri kama hawajaipa timu sapoti.

Shime amesema, anaamini ushindi upo kwani ameandaa kikosi kwa ajili ya kushindana na sio kushiriki japo wanakutana na timu kubwa kutoka kwa mataifa lakini anaamini ukubwa wa taifa haimaanishi kuwa na timu yenye ushindi mara zote.

Shime amesema, mashindano hayo yananafasi kubwa kwa upande wao na vijana wamewapa mafunzo kutokana na ubora wa timu watakazokutana nazo.

Timu ya Serengeti Boys inatarajia kuondoka hapo kesho jioni kuelekea nchini India kikiwa na msafara wa watu 28 kwa maana wachezaji 22 na viongozi sita kushiriki mashindano maalumu ya soka ya kimataifa kwa vijana (AIFF Youth Cup 2016 U-16) yaliyoandaliwa na Shirikisho la Soka nchini humo (AIFF).

Ratiba ya michuano inaonyesha kwamba Tanzania itafungua dimba na Marekani kwenye Uwanja wa Tilak Maidan, Vasco, Goa huku mchezo wa pili ukiwa kati ya wenyeji India dhidi ya Malaysia Mei 15, mwaka huu.

Serengeti Boys watashuka dimbani tena Mei 17, kucheza na wenyeji India mchezo wa kwanza, Mei 19 Serengeti Boys watacheza dhidi ya Korea Kusini na mchezo wa mwisho watamaliza dhidi ya Malaysia Mei 21 huku fainali ya michuano hiyo ikitarajiwa kuchezwa Mei 25 ambapo kabla ya mchezo wa fainali utachezwa mchezo wa mshindi wa tatu katika uwanja huo huo Tilak Maidan, Vasco, Goa.

Kupata nafasi ya kushiriki mashindano hayo maalumu ya vijana kimataifa ni sehemu ya maandalizi ya kikosi cha Serengeti Boys, kujiandaa na mchezo wa kuwania kufuzu kwa fainali za vijana barani Afrika dhidi ya Shelisheli Juni 25 hadi Julai 2 mwaka huu.