Peter amesema baada ya mwanae kupoteza nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha Simba ndipo akaamua kumwondoa na kumrejesha kwenye kituo chake cha kukuza vipaji vya makipa maarufu kama Tanzania Goal Keeping Training Centre.
“Ni kweli baada ya kumaliza mkataba wake Simba hatukutaka aendelee kwasababu hakuwa na nafasi ya kucheza hivyo tuliamua arejee kituoni aanze programu maalum kisha tumtafutie timu ndogo ili apate nafasi ya kucheza ndipo Singida wakakubali masharti wakamchukua”, amesema Manyika.
Mlinda mlango huyo mahiri wa zamani ameongeza kuwa kituo kilifanya kazi kubwa ya kurejesha makali ya Manyika Jr kuanzia kupunguza uzito pamoja na mbinu mbalimbali ambazo zimemsaidia golikipa huyo chipukizi kurudi kwenye kiwango bora akiwa na Singida United na sasa ameitwa Taifa Stars.

Manyika Jr alitamba na klabu ya Simba mwaka 2015 ambapo alifanikiwa kukaa langoni kwenye mechi ya Watani wa jadi Simba na Yanga na kuonesha kiwango kikubwa lakini alipoteza ubora msimu uliopita kabla ya kutimkia Singida United msimu huu ambako amerejea kuwa miongoni mwa magolikipa bora nchini.





