Saturday , 26th Jan , 2019

Afisa habari wa klabu ya Simba Haji Manara amefunguka kuchukizwa na kitendo cha mashabiki wa klabu hiyo kumtukana baada ya timu hiyo kupoteza nafasi katika michuano ya SportPesa Cup.

Afisa habari wa klabu ya Simba Haji Manara.

Manara ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na wanahabari leo Januari 26, ambapo amesema kuwa anasikitishwa na kitendo cha mashabiki hao kuingilia maisha yake binafsi.

"Nimechukizwa sana na mashabiki wa Simba kunitukana kwenye mitandao, kufikia hatua ya kunitukania mama mzazi kisa klabu kufungwa hawataki nifanye vitu vyangu binafsi, wanahoji kwanini nazindua bidhaa zangu wakati timu imefungwa", amesema Manara.

Ameongeza kuwa, "Haiwezekani kutofanya fanya shughuli zangu kisa Simba imefungwa, hiki ni kipato changu maana nina maisha yangu, waambieni kuwa sijawahi sema Simba nitaishi milele, nitabaki kuwa shabiki milele lakini sio kwenye kufanya kazi na tusichukuliane poa".

Baada ya Simba kutolewa na Bandari FC katika nusu fainali ya michuano ya SportPesa kesho itacheza na Mbao FC ili kusaka nafasi ya tatu.