Wednesday , 7th Jan , 2015

MICHUANO ya Kombe la Mapinduzi leo inaingia hatua ya Robo fainali kwa kuzikutanisha timu ya Simba SC na Timu ya Taifa Jang'ombe mechi inayotarajiwa kuchezwa uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Akizungumza na East Africa Radio, Katibu Mkuu wa Kamati ya maandalizi ya michuano hiyo, Khamis Said amesema, michuano hiyo ambayo ni maadhimisho ya miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar inatarajiwa kumaliza hatua yake ya Robo Fainali hapo kesho kwa kuzikutanisha mabingwa watetezi wa Kombe hilo KCCA na POLISI huku AZAM ikikutana na MTIBWA SUGAR na kumalizia kwa kuwakutanisha Yanga na JKU.

Said amesema nusu fainali za michuano hiyo inatarajiwa kuchezwa Januari 10 uwanja wa Amaan ambapo itawakutanisha mshindi kati ya Simba SC na Jang'ombe dhidi ya mshindi kati ya KCCA ya Uganda na Polisi ya Zanzibar, huku nusu fainali ya pili ikiwakutanisha mshindi kati ya Azam FC na Mtibwa Sugar dhidi ya mshindi kati ya Yanga na JKU.

Said amesema, michuano hiyo inatarajiwa kufikia Fainali Januari 13 ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.