
Habibu Kyombo akiwa na Mkurugenzi wa Singida United wakati wa utambulisho wake.
Taarifa kutoka katika klabu hiyo zinaeleza kuwa Habibu Kyombo alifanyiwa vipimo hivyo jana majira ya saa 7:00 mchana katika makao makuu ya klabu ya Mamelodi Sundowns nchini Afrika Kusini na sasa kinachoendelea ni makubaliano binafsi ya mchezaji na klabu hiyo.
"Tunamshukuru Mungu kwa hatua hii, hatua kubwa kwa klabu yetu na kubwa kwa mpira wa nchi yetu, Kyombo amefungua mlango, wengine wanafuata kupitia Singida United, kikubwa kujitambua na kuvumilia (Self determination)," imeeleza taarifa ya Singida United iliyotolewa katika mitandao ya kijamii.
Habibu Kyombo anakuwa mchezaji wa pili kwa Singida United kuuzwa nje ya nchi msimu huu, mchezaji wa kwanza ni Ally Hamis Ng'anzi aliyefuzu vipimo katika klabu ya MFK VySkov inayoshiriki ligi daraja la pili, nchi ya Jamhuri ya CZech.
Wakati huohuo Singida United kupitia kwa Mkurugenzi wake, Festo Sanga mapema hii leo imemtambulisha kinda, Viscon Mwale raia wa Zambia kwa mkataba wa miaka mitatu. Huyo anakuwa ni mchezaji wa tatu kusajiliwa hivi karibuni na klabu hiyo kutokea nchini Zambia, wengine waliosajiliwa ni pamoja na Gift Chikwangala na Jonathan Daka.