Wednesday , 5th Dec , 2018

Leo usiku majira ya saa 5:00 kutakuwa na mchezo wa kihistoria baina ya vigogo wawili wa ligi kuu nchini Uingereza, Man United na Arsenal, mchezo utakaopiogwa katika dimba la Old Trafford.

Nembo ya Manchester United na Arsenal

Timu hizi zina historia kubwa nchini Uingereza na bara la Ulaya hasa kuanzia miaka ya 1990' baada ya kuajiri makocha Arsene Wenger kwa upande wa Arsenal na Sir Alex Ferguson kwa upande wa Manchester United, ambao wameacha historia kubwa mpaka sasa.

Rekodi mbalimbali kuelekea mchezo huo

Manchester United haijafungwa katika mechi 11 za EPL za nyumbani dhidi ya Arsenal tangu mwezi Septemba mwaka 2006 ilipopoteza kwa goli 1-0. Katika mechi hizo 11, Man United imeshinda mechi 8 na kutoka sare mechi tatu.

Katika EPL, timu hizi zimekutana mara 178, Man United ikishinda mara 75 na Arsenal ikishinda mara 60 huku michezo 43 ikimalizika kwa sare. Ushindi mkubwa wa Arsenal dhidi ya Man United ni 4-0, mwezi Agosti mwaka 1970 na ushindi mkubwa wa Man United dhidi ya Arsenal ni 8-2, mwezi Agosti mwaka 2011.

Mchezo huu ni wa kwanza kwa Manchester United kuwa mwenyeji dhidi ya Arsenal katikati ya wiki tangu Mei 8, 2002 katika mchezo ambao ilipoteza kwa bao 1-0.

Ikumbukwe msimu uliopita Arsenal ilipoteza mechi tatu za mwisho ilizocheza katikati ya wiki (Jumanne, Jumatano na Alhamisi), ambapo mechi hizo zilikuwa dhidi ya timu za Swansea, Manchester City na Leicester City. Arsenal haijafungwa katika mechi 19 za mashindano yote ilizocheza msimu huu.

Kocha wa Arsenal, Unai Emery na kocha wa Manchester United, Jose Mourinho wamekutana mara 5, ambapo Jose Mourinho ameshinda michezo minne na mchezo mmoja ukimalizika kwa sare.

Katika msimu huu, Arsenal imeshinda mechi nne kati ya mechi sita ilizocheza ugenini huku ikipoteza mchezo mmoja na kutoka sare mchezo mmoja. Kwa upande wa Manchester United imecheza mechi sita katika uwanja wa nyumbani, ikishinda michezo mitatu, ikipoteza mchezo mmoja na kutoka sare michezo miwili.