Tuesday , 23rd Feb , 2016

Shirikisho linalopigana na matumizi ya dawa za kuongeza nguvu mwilini katika michezo (Wada), limesema juhudi za Kenya za kupambana na madawa ya kuongeza nguvu mwilini katika riadha hazitoshi.

Taarifa ya WADA imesema.''Hadi kufikia leo, rasimu ya sheria iliyopendekezwa na serikali ya Kenya na kamati iliyoundwa ili kupambana uenezi wa madawa hayo marufuku ya Kenya, kwa hakika haiafikiani kabisa na kanuni za WADA''.

WADA imeipa Kenya muda hadi Aprili 5 kuhakikisha imeainisha sheria zake na kanuni zote za kupambana na madawa yaliyopigwa marufuku.

Waziri wa michezo wa Kenya bwana Hassan Wario aliiahidi WADA kuwa mapendekezo ya sheria hiyo ya kupambana na matumizi ya madawa yatajadiliwa bungeni na kupitishwa kesho.

Onyo hilo la WADA linatia wasiwasi kwa maelfu ya mashabiki wa riadha nchini Kenya kwani Rais wa shirikisho la riadha duniani Lord Sebastian Coe alikuwa ameonya kuwa hatachelea kuipiga marufuku Kenya kutoshiriki mashindano ya Olimipiki yatakayoandaliwa mjini Rio de Jenairo Brazil mwezi Agosti mwaka huu.

Kenya ndiyo taifa bingwa wa medali za riadha duniani na kama itafungiwa kushiriki Olympic basi itakuwa furaha kwa mataifa pinzani.
Hadi kufikia sasa takriban wanariadha 40 wamepatikana na hatia ya kutumia madawa yaliyopigwa marufuku michezoni.