Monday , 22nd Jan , 2018

Mabingwa watetezi wa ligi kuu soka Tanzania Bara Yanga SC, wamesema wachezaji Oscar Mkomola na Pius Buswita ni wazima tofauti na taarifa zinazosambazwa kuwa wameumia na watakosa mchezo dhidi ya Azam FC.

Msemaji wa klabu hiyo Dismas Ten amesema nyota hao wanaendelea vizuri na wamerejea mazoezini kwasababu hawakuumia sana jana ilikuwa ni mgongano wa kawaida kwenye mchezo wa soka.

''Daktari amesema Mkomola na Buswita ni wazima na wanaendelea na programu za mazoezi, hawakuumia sana jana ilikuwa ni migongano ya kawaida hivyo wako sawa na wanajiandaa na mchezo wa ligi ujao dhidi ya Azam FC'', amesema Dismas.

Buswita ambaye amesajiliwa msimu huu akitokea Mbao FC, jana alifunga bao pekee lililowapa ushindi Yanga dhidi ya Ruvu Shooting kwenye mchezo uliopigwa uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam. Mkomola pia amesajiliwa msimu huu baada ya kufanya vizuri na kikosi cha Serengeti Boys.

Yanga ambayo inashika nafasi ya tatu ikiwa na alama 25 itashuka dimbani jumamosi kukipiga na Azam FC kwenye mchezo wa raundi ya 15.