Thursday , 29th Nov , 2018

Klabu ya Yanga imefanikiwa kukaa kileleni mwa ligi kuu Tanzania bara, baada ya kuichapa mabao 3-0 JKT Tanzania katika mchezo wa ligi kuu Tanzania bara katika uwanja wa taifa jijini Dar es salaam.

Yanga (kushoto) na Man City (kulia)

Mchezo huo wa 13 kwa upande wa Yanga, ulimalizika kwa kalamu nzuri ya mabao yaliyofungwa na Heritier Makambo katika dakika ya 20, Mrisho Ngassa dakika ya 53 na Ibrahim Ajibu katika dakika ya 79 kwa mkwaju wa penati.

Baada ya kumalizika kwa mchezo huo, sasa Yanga inafikisha alama 35 zinazoipeleka kileleni mwa msimamo wa ligi kuu, ikiipiku Azam FC yenye alama 33 huku Simba ikisalia katika nafasi ya tatu kwa alama 27.

Alama hizo 35 za Yanga pia zinapelekea kuwa sawa na bingwa mtetezi wa ligi kuu nchini Uingereza EPL, Manchester City mwenye alama hizo baada ya kushuka dimbani katika michezo 13, ikishinda mechi 11, sare mbili huku ikiwa haijafungwa mechi yoyote.

Endapo Manchester City itafanikiwa kunyakuwa ubingwa wa EPL msimu huu, itakuwa imeweka rekodi ya kushinda mara mbili mfululizo au zaidi tangu msimu wa 2006/07 hadi 2008/09 Manchester United ilipofanya hivyo. Huku katika ligi kuu Tanzania bara, Yanga ikiwa ndiyo klabu pekee iliyoweka rekodi hiyo katika miaka ya karibuni, ikifanikiwa kushinda ubingwa wa ligi mara tatu mfululizo tangu msimu wa 2014/15 hadi 2016/17.