Thursday , 20th Dec , 2018

Nahodha wa Yanga, Kelvin Yondani ameweka wazi kuwa katika kipindi hiki ambacho hali ya klabu hiyo haiko sawa kiuchumi, ameshuhudia upendo wa dhati kutoka kwa mashabiki ambao wamekuwa wakiwachangia pesa.

Kelvin Yondani akifanyiwa mahojiano

Akiongea kupitia mtandao wa Yanga, nahodha huyo amesema wamekuwa wakipata motisha ya kujituma zaidi kutokana na kiasi kidogo cha fedha ambacho kimekuwa kikitoka kwa mashabiki moja kwa moja na kuwafikia wao hususani siku za mechi.

“Tunapopata hicho kiasi kidogo kutoka kwa mashabiki wetu, hakika kinatuongezea hamasa kubwa ya kupambana zaidi, tunawashukuru sana,” amesema Yondani.

Yondani ambaye yupo jijini Arusha na kikosi cha Yanga kitakachocheza mchezo wa ligi kuu soka Tanzania bara dhidi ya African Lyon leo kwenye uwanja wa Sheikh Abeid Karume ameongeza kuwa wamekuwa wakipokea fedha kutoka kwenye makundi mbalimbali ya mashabiki wa Yanga kwenye mitandao ya kijamii.

''Muda mwingine wanatupatia fedha mabazo kwa kuziona ni kidogo lakini zina thamani kubwa sana kwetu na ndio maana tunajituma uwanjani ili tupate matokeo na wao wafurahi wazidi kutuunga mkono zaidi na zaidi'', ameongeza Yondani.