Monday , 11th Jan , 2016

Baada ya kutolewa katika michuano ya kombe la Mapinduzi, Kikosi cha timu ya Simba SC kimeendelea kujichimbia visiwani Zanzibar kwa ajili ya maandalizi ya muendelezo wa michuano ya ligi kuu ya soka Tanzania Bara itakayoendelea Januari 16 mwaka huu.

Afisa habari wa Simba SC Hajji Manara amesema, timu inatarajiwa kuwasili jijini Dar es salaam siku ya Alhamisi ya Januari 14 mwaka huu kwa ajili ya maandalizi ya mechi ya ligi kuu dhidi ya Mtibwa Sugar itakayopigwa uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

Manara amesema, wameona ni vizuri kubaki Zanzibar kutokana na utulivu uliopo kwa ajili ya kuwajenga wachezaji kwa ajili ya kuchukua pointi tatu na hawatakuwa tayari kupoteza tena mchezo dhidi ya Mtibwa.

Manara amesema, wanaamini kwa kumuongeza katika benchi la ufundi kocha Jackson Mayanja ambaye ni kocha msadizi itasaidia kuendelea kukijenga kikosi katika michuano ya ligi kuu.