
Akiongea na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Daktari Bingwa wa ugonjwa wa Saratani kutoka taasisi binafsi ya TASOI, Dkt. Kweka Walter amesema kati ya watanzania100,000, 100 kati yao wana saratani na kushauri jamii kupima zaidi saratani aina shingo ya kizazi, tezi dume na ya matiti ambayo huathiri watu wengi zaidi nchini.
"Si sawa kuiachia serikali jukumu lote la kulinda afya zetu bila sisi wenyewe kuchukua hatua namba moja, kila mtu ni muathirika mtarajiwa wa saratani sasa, kwanini tusijali afya zetu kwa kupima, ukipima mapema na kugundulika katika hatua za awali basi utafanikiwa sana," amesema Dkt. Kweka.
Aidha, Dkt. Kweka, amewataka wanawake wa kuanzia umri wa miaka 18 na kuendelea kuepuka ngono zembe ili kuepuka kupata Saratani ya Shingo ya Kizazi inayopelekea vifo vya wanawake elfu 4,216 nchini kwa mwaka, kwa kuwa asilimia 69 ya wanawake nchini wana virusi vinavyo pelekea ugonjwa huo.