Wednesday , 5th Oct , 2016

Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma wa Chama cha Wananchi (CUF), Abdul Kambaya amesema kwamba mgogoro unaoendelea ndani ya chama hicho utamalizwa na wanachama na viongozi wa chama hicho pekee na siyo kuingiliwa na viongozi wa UKAWA.

Abdul Kambaya, ambaye pia ni miongoni mwa wanachama wa CUF waliosimamishwa

Kambaya ameyasema hayo katika kipindi cha East Africa Break Fast na kusisitiza kwamba mgogoro huo utaisha kwa pande zote kukaa chini na kujadili mustakabali wa chama chao na siyo watu wengine kuwaingilia kufanya maamuzi.

“Tutafanikiwa kuvuka mgogoro huu kama tutakaa chini kwa pamoja, tuzungumze na kuelewana lakini kama watu wengine wakiingilia na upande mmoja ukawaamini hatutafikia mwisho na wanachama watazidi kugawanyika” Amesema Kambaya

Mgogoro wa CUF umezidi kushika kasi baada ya Baraza Kuu la chama hicho lililoketi Zanzibar kutangaza kumvua uanachama Prof. Ibrahim Lipumba kwa ukiukaji wa katiba ya chama hicho huku Ofisi ya Msajili wa Vyama Vya Siasa ikitangaza kumtambua Prof. Lipumba kama Mwenyekiti halali wa chama hicho.