Tuesday , 13th Nov , 2018

Shirikisho la soka nchini TFF kupitia Kamati ya Maadili, limewafungia Mwenyekiti wa matawi wa klabu ya Yanga, Bakili Makele na katibu wa matawi wa klabu hiyo Boaz Ikupilika kutojihusisha na soka kwa kipindi cha miaka mitatu kwa kukaidi maamuzi ya serikali na shirikisho hilo.

Hamidu Mbwezeleni

Maamuzi hayo yametolewa hii leo na Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya TFF, Hamidu Mbwezeleni katika mkutano na wanahabari uliofanyika katika ofisi za shirikisho hilo, Ilala jijini Dar es salaam.

Viongozi hao wanadaiwa kupinga maagizo ya serikali na TFF ya kufanya uchaguzi wa kujaza nafasi ambazo ziko wazi ndani ya klabu ya Yanga.

Pamoja adhabu hiyo waliyopewa, pia wanatakiwa kulipa faini ya shilingi milioni 2 kila mmoja.
Hivi karibuni Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania(TFF) kupitia Mwenyekiti wake, Malangwe Mchungahela ilitangaza tarehe ya uchaguzi wa klabu ya Yanga ambayo ni Januari 13, 2019 na kuiagiza klabu hiyo kuanza mchakato wa kutoa fomu za wagombea mara moja.

Nafasi zitakazogombewa katika klabu hiyo ni pamoja na nafasi ya Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Wajumbe wanne wa kamati ya utendaji.