Thursday , 12th Dec , 2019

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Wankyo Nyigesa, amesema kuwa Jeshi la Polisi mkoani humo linamshikilia Mustafa Malimi (25) ambaye juzi Desemba 9, 2019 alipata msamaha wa Rais Magufuli na kuachiwa huru kwa kosa la kuiba Ng'ombe mwenye thamani ya Shilingi milioni 1.2.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Wankyo Nyigesa.

Akizungumza leo Desemba 12, 2019, Kamanda Wankyo amesema kuwa Mustafa alifanya kosa hilo Desemba 10 na jana Desemba 11, majira ya saa 4:00 asubuhi, maeneo ya Nero Magorofani, katika Wilaya ya Chalinze, walimkamata tena kwa kosa ambalo hapo awali lilimfunga miezi sita gerezani.

"Huyu juzi tu amepata msamaha wa Rais na tumemkamata tena muda mfupi baada ya kuachiwa huru, awali alikuwa ni mfungwa kwenye Gereza la Ubena na jana tumemkamata akiwa ameiba Ng'ombe na kosa la awali lililokuwa limemfunga ni la wizi wa Mbuzi na alihukumiwa miezi sita kwenda jela" amesema Kamanda Wankyo.

Kamanda Wankyo ameongeza kuwa Jeshi la Polisi bado linaendelea kumshikilia na baada ya hapo watampeleka mahakamani kwa kosa la wizi wa mifugo.