Wednesday , 15th Jan , 2020

Kuelekea mchezo wa Ligi kuu soka Tanzania Bara kesho Alhamis 16, 2020, klabu ya soka ya Mbao FC imesema imejiandaa vizuri licha ya wapinzani wao Simba kuwa na kila kitu kinachoweza kuwapa ushindi.

Kushoto ni Haji Manara na kulia ni wachezaji wa Mbao FC

Akiongea na EATV & EA Radio Digital, kocha msaidizi wa Mbao FC Abdulmutik Hajji ameweka wazi kuwa wamefanya maandalizi yao vizuri kwa kuzingatia ubora wa wapinzani wao.

'Tumejiandaa vizuri kuelekea mchezo wa ligi kuu kesho dhidi ya Simba lakini tunaiheshimu Simba kutokana na uzoefu mkubwa ilionao', amesema Hajji.

Kwa upande wa msemaji wa Simba Haji Manara amesema wanataka kupata pointi zote 6 za michezo miwili ya Mwanza ambayo ni dhidi ya Mbao FC na Alliance FC.

'Sasa akili yetu tuelekeze Mwanza katika mechi mbili ngumu zijazo, tushirikiane kupata pointi sita za CCM Kirumba, Insha'Allah tutafanikiwa', ameandika Manara.

Msimu huu Mbao FC wamecheza mechi 16 ambapo wameshinda mechi 4, Sare 6 na kufungwa mechi 6, wakati Simba wamecheza mechi 14, wameshinda 11, sare 2 na kufungwa 1.

Katika dirisha dogo la usajili Mbao FC wamesajili wachezaji watatu ambao Omary Wayne kutoka Ndanda SC walinzi Hussein Iddi kutoka Mtibwa Sugar na Mackyada Franco kutoka Coastal Union.

Simba wao wamesajili mchezaji mmoja ambaye ni Luis Miquissone kutoka UD Songo ya Msumbiji.