Sunday , 26th Jan , 2020

Serikali mkoani Morogoro imesikitishwa na mwendo wa kusuasua wa ujenzi wa barabara ya Kidatu-Ifakara baada ya miundombinu iliyopo kushindwa kustahimili maji mengi, mkandarasi akiwa amefikia asilimia 10 pekee huku mradi ukitarajiwa kukabidhiwa Aprili mwaka huu.

Eneo la Kanolo ambalo daraja limesombwa na maji

Hayo yamebainishwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoani humo ilipotembelea mradi huo ikiongozwa na Katibu Tawala wa mkoa, Mhandisi Emmanuel Kalobelo kufuatia daraja lililopo eneo la Kanolo wilayani Kilombero kusombwa na maji usiku wa Januari 24 kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha.

Mkuu wa Wilaya ya Kilombero na Wakala wa Barabara mkoani Morogoro wamesema hawaridhishwi na kasi ya ujenzi wa mradi huo kwani mpaka sasa mkandarasi yuko nyuma ya muda kwa asilimia 90.

Naye Mhandisi Mshauri katika mradi huo, Maburugi Mapambano amekiri kuwa mradi huo uko nyuma huku wananchi wakiiomba serikali iangalie uwezekano wa kubadilisha mkandarasi huyo.