Wednesday , 15th Jul , 2020

Patashika ya ligi kuu Tanzania bara raundi ya 35 itaendelea leo kwa mitanange 6 kupigwa ambapo klabu ya Namungo ambao wapo katika nafasi ya 4 na alama zao 60,wataialika Mbeya City iliyo katika nafasi ya 16 na alama zake 39 mchezo huo utapigwa katika uwanja wa Majaliwa.

Mlinzi wa Yanga Juma Makapu akimvuta nyota wa Azam Fc, Never Tegere katika mchezo wa ligi kuu Tanzania Bara.

Mchezo mwingine utapigwa uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma ambapo JKT Tanzania iliyo katika nafasi ya 7 kwa alama zao 48,wataialika Alliance kutoka Mwanza ambayo  ipo nafasi ya 15 wakiwa na alama 40.

Shughuli pevu nyingine itakua katika uwanja Kaitaba mjini Bukoba ambapo wanankurukumbi Kagera Sugar wakiwa nafasi ya 9 na alama zao 46,itakua mwenyeji wa Maangushi Coastal Union kutoka Tanga ambao hadi sasa wapo nafasi ya 5 wakiwa na alama zao 51.

Huko Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara, Ndanda ya kocha meja mstaafu Abdul Mingange iliyo katika mstari wa kushuka daraja ambayo ni nafasi ya18 na alama 37 itakabiliana na Tanzania Prisons kutoka Mbeya ambayo ipo nafasi ya 11 na alama zao 44.

Macbingwa wa zamani mwaka 1999 na 2000 ,Mtiwa Sugar ambao wapo nafasi ya 17 na alama zao 38 watakua na kibarua kizito mbele ya Azam ambayo inahitaji kujikita katika nafasi ya pili waliyopo hivi sasa kwa alama zao 65.

Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam klabu ya Yanga itakua ikihitaji kuwapa angalau faraja mashabiki wake baada ya kupokea kipigo cha fedheha siku ya jumapili dhidi ya Simba katika FA,itaikaribisha Singida United ambayo imeshashuka daraja.