Thursday , 6th Aug , 2020

Rais Dkt. John  Magufuli leo Agosti 6, 2020, amefika katika ofisi za NEC na kuchukua fomu ya kugombea nafasi ya urais wa  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kuchaguliwa na chama cha mapinduzi  CCM kuwania nafasi hiyo.

Rais Magufuli na Mgombea Mwenza Samia Suluhu wakichukua fomu

Rais Magufuli anakuwa ni mgombea wanne kuchukua fomu ambapo kwa siku ya jana wagombea kutoka vyama vya  AAFP, DP na NRA walifika katika ofisi za NEC wakiwa na wagombea wenza kwa ajili ya kukamilisha zoezi hilo.

Kwa mujibu wa  Mchambuzi Mkuu  wa Siasa Samson Charles kutoka East Africa Television na East Africa Radio, ametoa maoni yake katika kipindi cha The Drive Show kinachoruka kila siku za wiki kuanzia Saa 10:00 Jioni hadi Saa 2:00 Usiku, ambapo amedai kuwa kwa mwaka huu joto la kisiasa linakolea na kuna ushindani mkubwa ambapo hadi sasa vyama vingine bado vinaendelea na vikao, na kwa upande wa CHADEMA mgombea wao atachukua fomu siku ya Agosti 8.

“Joto la uchaguzi linakolea kabla hata kampeni hazijaanza tarehe 26 mwezi huu, uchukuaji fomu umeanza rasmi siku ya jana  na utakwenda hadi tarehe 25 mwezi huu,nimezungumza na vyama vingine bado wako kwenye vikao, huenda tukawa na uchaguzi wenye ushindani mkubwa labda kuliko watu walivyokuwa wakitegemea”. Amesema Samson Charles

Tafiti zinaonesha watu waliojiandikisha katika daftari la kudumu la kupiga kura ni zaidi ya watu milioni 23 kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na vyama ambavyo vitashiriki uchaguzi huo ni 19.