Thursday , 20th Aug , 2020

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli, amesema kuwa amehesabu na kusoma majina yote ya wagombea wa nafasi ya Ubunge kwa lengo la kuhakikisha wanawajadili kwa kina ili kujiridhisha kam wote watakaowapitisha wanazo sifa na uwezo wa kuongoza.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo hii leo Agosti 20, 2020, wakati wa ufunguzi wa Kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, unaofanyika Jijini Dodoma, ambapo ameongeza kuwa lengo lingine ni kupata viongozi wenye utayari wa kuwatumikia wananchi.

"Ndugu zangu juzi na jana majina ya wagombea yalijadiliwa kwenye vikao kwa ajili ya uchambuzi wa kina, napenda niwahakikishie kuwa tulitumia taarifa nyingi ambazo tulizipata kutoka katika vyanzo mbalimbali na mimi nataka kuwathibitishia Wabunge, nimesoma majina yote 10,367 na ndiyo maana uchambuzi wa kila mmoja tunao hapa kwa yule atakayetaka ufafanuzi wa mtu yoyote", amesema Rais Magufuli.

Aidha Rais Magufuli ametoa wito kwa Wajumbe kuwa Ukanda, Undugu na Ukabila uwekwe pembeni katika upitishaji wa majina ya wagombea hao na badala yake watangulize maslahi ya Watanzania na chama kiujumla.