Tuesday , 10th Nov , 2020

Nahodha na mshambuliaji tegemeo wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mbwana Samatta atakosekana katika mechi ijayo dhidi ya Tunisia ambayo ni ya kufuzu fainali za mataifa ya Afrika mwakani kufuatia kupata majeraha ya nyama za paja.

Nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta akishangilia bao alilofunga dhidi ya Harambee Stars katika michuano ya AFCON,2019 iliyofanyika nchini Misri.

Nyota huyo ambaye kwasasa anakipiga katika klabu ya Fenerbahce ya Uturuki, alitembelea kambi ya Stars jana kuzungumza na kocha mkuu Etienne Ndayiragije na wachezaji kuwapa hamasa kabla ya kuivaa Tunisia Novemba 13 mwaka huu.

Akizungumzia masikitiko yake kufuatia kukosekana kwake, Samatta amesema''Nasikitika kukosekana katika mchezo wa timu yangu ya Taifa ninayoipenda, malengo yangu ni kutoa mchango wangu lakini daktari wa klabu yangu ameniambia nitahitaji kupumzika siku 10 ili niweze kupona maumivu niliyonayo.Niliumia katika mchezo tuliopoteza dhidi ya Konyaspor hivyo naumia kukosa nafasi ya kucheza dhidi ya Tunisia''.

Taifa Stars ipo kambini nchini Uturuki na itakabiliana na Tunisia Novemba 13 kabla ya kurudiana na miamba hiyo ya Afrika wiki moja baadaye hapa nchini Tanzania.