Tuesday , 17th Nov , 2020

Kiungo wa timu ya taifa ya Tanzania, Salum Aboubaka 'Sure boy' ataukosa mchezo wa leo wa kufuzu michuano ya mataifa ya Afrika dhidi ya Tunisia kufuatia kupata majeruhi.

Kocha wa Taifa Stars, Etienne Ndayiragije akizungumzia matayarisho ya mchezo dhidi ya Tunisia.

Kocha wa Taifa Stars, Etienne Ndayiragije ndiye aliyethibitisha kukosekana kwa nyota huyo ambaye alikuwa na mchezo mzuri katika mchezo uliopita ambao Tanzania ilifungwa bao 1-0.

''Tulifanya mazoezi ya mwisho kujiweka vizuri kabla ya mchezo, hali sio mbaya lakini kiafnya tutamkosa Sure boy ambaye ni majeruhi .Lakini wachezaji wengine wazima, Adam Adam ambaye alikosekana katika mechi iliyopita kutokana na kuchelewa kwa hati ya kusafiria leo atarejea hivyo tupo imara'' alisema Ndayiragije.

Stars ilifanya mazoezi ya mwisho kabla jana na leo saa nne usiku watakabiliana na Tunisia katika mchezo wa kundi J ambao pia umebeba taswira ya timu zitakazofuzu katika michuano ya Afcon mwakani.

Kundi J linaongozwa na Tunisia yenye alama tisa katika mechi tatu, wakati Equatorial Guinea ikishika nafasi ya pili wakiwa na alama 6, Libya na Taifa Stars zikifuatia katika nafasi ya tatu na ya nne zikiwa na alama tatu kila mmoja.