Tuesday , 24th Nov , 2020

Ofisi ya utawala wa huduma za serikali nchini Marekani, imemtaarifu Rais mteule wa Marekani, Joe Biden, kwamba Rais Donald Trump, anayemaliza muda wake yupo tayari kwa ajili ya kuanza mchakato rasmi wa kukabidhiana madaraka.

Rais Mteule wa Marekani, Joe Biden

Kwa mujibu wa barua kutoka kwa msimamizi katika ofisi ya utawala wa huduma za serikali, Emily Murphy, iliyotumwa siku ya Jumatatu imeweka wazi kumtambua rasmi Joe Biden, kama Rais mteule wa Marekani huku akidai kuwa uamuzi huo ni kwa mujibu wa sheria .

“Sikushinikizwa moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja na afisa yeyote mtendaji ofisi ya utawala wa huduma za serikali, pamoja na wafanyakazi wa Ikulu na sikupokea mwelekeo wowote wa kuchelewesha uamuzi wangu” aliandika Emily kwenye barua yake

Barua hiyo inaashiria rasmi juu ya ushindi wa Joe Biden, na hatua hiyo itaruhusu mchakato wa mabadiliko kuanza rasmi huku timu ya Biden, ikiwa imefurahishwa na kuanza kwa mchakato huo wakati rais mteule anajiandaa katika sherehe za kuapishwa Januari 20, 2021.

Mapema Jumatatu, Joe Biden, alizindua timu itakayoangazia sera ya fedha na usalama wa taifa, iliyojumuisha watu wa zamani wa miaka hiyo katika utawala wa Obama.