
Mauricio Pochetino aliichezea PSG kati ya mwaka 2000-2003, na sasa anatajwa kuwa amesaini mkataba wakuwa kocha wa klabu hiyo
Hatua hii inakuja baada ya kocha wa zamani wa timu hiyo Thomas Tuchel kufikia makubaliano ya kuvunja mkataba.
Klabu ya PSG imeripotiwa kufikia makubaliano ya kuvunja mkataba na Thomas Tuchel ambaye watamlipa fidia ya peza za Uingereza pauni milion 5.4, ambayo ni zaidi ya bilion 15 za kitanzania. Tuchel alifutwa kazi siku ya Jumatano Disemba 23, usiku, saa chache baada ya kukiongoza kikosi hicho kupata ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Racing Strasbourg kwenye mchezo wa ligi kuu.
Baada ya matajiri hao wa jiji la Paris kumalizana na kocha huyo raia wa Ujerumani, imeripotiwa kuwa wameshaingia makubaliana na Mauricio Pochetino, ambaye aliwahi kuichezea klabu hiyo kati ya mwaka 2000-2003, ingawa taarifa hizo hazijawekwa wazi amesaini mkataba wa miaka mingapi.
Pochettino amekuwa hana timu tangu alipoachana na Tottenham mwaka jana. Muargentina huyo mwenye umri wa miaka 48, amekuwa akihusishwa kujiunga na vilabu kadhaa ikiwemo FC Barcelona, Real Madrid na Manchester United.