
Aliyewahi kuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Marehemu Balozi Dkt. Augustine Mahiga.
Balozi Dkt. Mahiga, ambaye aling'ara kwenye duru za kimataifa tangu ujana wake, alifariki dunia akiwa nyumbani kwake jijini Dodoma, baada ya kuugua ghafla na wakati anafikishwa hospitali, alikuwa tayari amekwishapoteza maisha, na Tanzania ilipokea salamu za pole na rambirambi kutoka katika kila pembe ya nchi na kutoka mataifa mbalimbali Duniani.
Wakati wa uhai wake, marehemu Dkt. Mahiga, aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya nchi na kimataifa, ambapo kwa miaka mingi alikuwa mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, ambapo akiwa katika chombo hicho cha kimataifa, alishiriki kikamilifu katika michakato ya kusaka amani katika eneo la nchi za maziwa makuu na nyinginezo za Afrika.
Marehemu Balozi Dkt. Mahiga, pia aliwahi kuwa mwakilishi wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon nchini Somalia, ambako alisaidia kuleta utangamano katika Taifa hilo.
Mbali na hayo marehemu Balozi Dkt. Mahiga, alikuwa ni kiungo muhimu kati ya Tanzania na Mataifa ya Magharibi wakati alipokuwa akitekeleza majukumu yake kama Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, baada tu ya kuapishwa kwenye wadhifa huo mwaka 2015, na Rais Dkt. John Magufuli, ambapo mpaka umauti unamfika alikuwa ni Waziri wa Katiba na Sheria.
Kwa kipindi cha miaka 30 kutoka mwaka 1983 mpaka 2013, marehemu Balozi Dkt. Mahiga, alifanya kazi ya diplomasia akiiwakilisha Tanzania kama Balozi na pia kuwakilisha Umoja wa Mataifa (UN) katika nchi mbalimbali.
Kwa miaka sita kutoka 1983 mpaka 1989 alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Canada na kutoka 1989 hadi 1992, akahudumu katika ubalozi wa kudumu wa Tanzania katika ofisi za UN jijini Geneva, Uswisi.
Kutoka mwaka 1992 mpaka mwaka 1994, alihudumu kama mwakilishi mkaazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Wakimbizi (UNHCR) nchini Liberia na kutoka 1994 mpaka 1998 alirudi Geneva na kuwa mratibu na Mkurugenzi Msaidizi wa Oparesheni za Dharura za Wakimbizi, katika eneo la Maziwa Makuu Barani Afrika.
Kutoka 1998 mpaka 2002, marehemu Balozi Dkt. Mahiga, alikuwa mwakilishi mkaazi wa UNHCR India, na kutoka 2002 mpaka 2003, alikuwa ni mwakilishi wa shirika hilo katika nchi za Italia, Malta na San Marino.
Mwaka 2003 aliteuliwa na Rais wa awamu ya tatu marehemu Benjamin Mkapa, kuwa Balozi wa Tanzania katika Ofisi za kudumu za Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa (UN) jijini New York, na kusalia katika nafasi hiyo katika muhula wa kwanza wa Rais wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Kikwete hadi 2010.
Licha ya utajiri wake wa maarifa na uzoefu mkubwa ndani na nje ya Tanzania, Balozi marehemu Dkt. Mahiga, alikuwa mtu ambaye hakujikweza kwa mamlaka yake na hiyo ni mojawapo ya sifa ambayo watu waliokuwa wakimuomboleza walimpamba nayo.
Marehemu Balozi Dkt. Mahiga, alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 74 na kuzikwa Mei 2, 2020, kijijini kwao katika makaburi ya Tosamaganga mkoani Iringa, ambapo katika shughuli ya maziko yake, Rais Dkt. Magufuli, aliwakilishwa na Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu.