Monday , 4th Jan , 2021

Kocha wa FC Barcelona Ronald Koeman ameweka wazi kuwa anahitaji kusajili mshambuliaji kwenye dirisha dogo la mwezi Januari, baada ya kikosi cha kuibuka na ushindi wa bao 1 - 0, dhidi ya Huesca kwenye mchezo wa ligi licha ya timu hiyo kupiga mashuti 11 yaliyolenga lango.

Ronald Koeman ameweka wazi kuwa anahitaji mshambuliaji kwenye dirisha dogo la usajili

Licha ya ushindi huo lakini kocha Koeman hakuridhishwa na kiwango cha wachezaji wake wa safu ya ushambuliaji, ambayo iliongozwa na Ousmane Dembele, Martin Braithwaite na Lionel Messi.

Baada ya mchezo huo, Koeman alisema anamuamini kila mchezaji lakini anahitaji mchezaji mshindani na mwenye uwezo wa kufunga.

"Hakuna haja ya kurudia kile tulichosema mwanzoni mwa msimu, kwamba tunahitaji mtu kwenye ushambuliaji ili kuwa na ushindani zaidi, magoli zaidi na ufanisi zaidi, lakini inategemea na mambo mengi," alisema Koeman.

Msimu huu kwenye michezo 16 ya ligi kuu Hispania La Liga, Barcelona wamefunga mabao 30 ambao ni wastani wa bao 1.87 kwa mchezo huko wao wakiwa wameruhusu mabao 15 kwenye wavu wao. Lionel Messi ndio kinara wa ufungaji wa Barca kwenye michezo ya ligi akiwa na mabao 7 akifatiwa na Ansu Fati mwenye mabao 4.

Frenkie De Jong alifunga bao hilo pekee la Barcelona licha ya kikosi hicho kuwa na umiliki wa mpira wa asilimia 70 na kupiga mashuti 11 yaliyolenga goli. Barcelona ipo nafasi ya 5 ikiwa na alama 28.