
Simba wanahitaji ushindi wowote wa tofauti ya mabao kuanzia 2 ili kujihakikishia nafasi ya kutinga hatua ya makundi.
Huu ni mchezo wa mkondo wa pili ikiwa ni mchezo wa raundi ya kwanza wa michuano ya klabu bingwa Afrika, Wenyeji Simba wanahitaji ushindi wa kuanzia mabao 2-0 au ushindi wowote wa tofauti ya mabao kuanzia 2 ili kujihakikishia nafasi ya kutinga hatua ya makundi.
Wachimba madini wa Zimbabwe FC Platinum wanaingia kwenye mchezo wa leo wakiwa na faida dhidi ya wenyeji wao wekundu wa msimambazi Simba SC, kwa faida ya kuongoza kwa bao 1-0, ushindi ambao waliupata kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza ambao ulipigwa mjini Harare Nchini Zimbabwe, bao la pekee kwenye mchezo huo lilifungwa na Perfect Chikwende dakika ya 17.
Wachezaji watakaokosekana kwa upande wa Simba ni Jonas Mkude, ambaye amesimamishwa kutokana na utovu wa nidhamu, mchezaji mwingine ni Bernard Morrison ambaye pia aliukosa mchezo wa kwanza kwa kuwa alikuwa anaumwa.
Kocha wa FC Platinum Norman Mapeza amesisitiza kuwa lengo lao ni kamaliza kazi waliyoianza kwenye mchezo wa kwanza, ikiwa ni kuhakikisha wanaibuka na ushindi kwenye mchezo huu, wakati kocha wa Simba Sven Vandenbroeck, anaamini watapindua matokeo na watafuzu hatua ya makundi.
Mgeni rasmi kwenye mchezo huo utakaopigwa kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa, Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Simba SC dhidi ya FC Platinum atakuwa ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro.