Friday , 22nd Jan , 2021

Mabingwa watetezi wa EPL, klabu ya Liverpool imefungwa bao 1-0 dhidi ya Burnley usiku wa kuamkia leo na Burnley wamevunja rekodi ya Liverpool kucheza michezo 68 ya EPL bila kufungwa kwenye uwanja wake wa nyumbani, uwanja wa Anfield.

Mshambuliaji wa Burnley, Ashley Barnes akifunga bao na kuwapa ushindi Burnley wa 1-0 dhidi ya Liverpool usiku wa jana.

Mshambuliaji wa Burnley, Ashley Barnes ndiye aliyeandika historia hiyo baada ya kufunga bao dakika ya 83 kwa penalty kufuatia muamuzi wa kati Mike Dean na jopo la waamuzi wa VAR wa mchezo huo kukubaliana mlinda wa Liverpool Alisson Becker alimkwatua Barnes.

Mara ya mwisho Liverpool kufungwa kwenye dimba  lake la nyumbani la Anfield kwenye EPL, ilikuwa ni tarehe 23 Aprili 2017 walipofungwa mabao 2-1 dhidi ya Crystal Palace na bao la ushindi kwenye mchezo huo lilifungwa na mchezaji wao wazamani Christian Benteke.

Baada ya rekodi hiyo kuvunjwa, Kocha wa sasa wa Tottenham Hotspurs ya Uingereza, Jose Mourinho atakuwa mwenye furaha kwasababu Liverpool ilikuwa inasaka rekodi ya Chelsea kutofungwa kwenye uwanja wake wa nyumbani ‘Stamford bridge’ kwa kucheza michezo 86.

Rekodi hiyo ya Chelsea iliwekwa kuanzia mwaka 2004 Aprili hadi Oktoba 2008 na kocha Jose Mourinho, na ndiyo rekodi inayoshikilia namba moja kwa timu kucheza michezo mingi zaidi kwenye uwanja wake wa nyumbani bila kufungwa kwenye EPL.

Kuondoa rekodi ya Liverpool kufungwa Anfield, lakini imeweka rekodi ya kucheza michezo mitano bila kupata ushindi kwa mara ya pili, mara ya kwanza ilikuwa mwezi Januari hadi Februari mwaka 2017 chini ya kochwa Jurgen Klopp.