Sunday , 21st Feb , 2021

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Aboubakar Kunenge amesema ifikapo Alhamis ya Februari 25 kituo kipya cha mabasi yaendayo mikoani na nje ya nchi cha Mbezi Luis kitaanza rasmi kutoa huduma na kituo mabasi Ubungo kilichokuwa kikitumika awali hakitotumika tena.

Pichani muonekano wa kituo cha kipya cha mabasi yaendayo mikoani na nje ya nchi cha Mbezi Luis.

RC Kunenge amesema hatua hiyo imekuja baada ya kukamilika kwa miundombinu yote muhimu ikiwemo majengo, maegesho, barabara na ofisi za kutoa huduma.\

                                     Muonekano wa kituo cha mabasi Mbezi Luis

Aidha, RC Kunenge amesema tayari Serikali imekutana na wadau wote husika ikiwemo chama Cha Wamiliki wa Mabasi TABOA na wote wamejiridhisha kuwa kituo kimekamilika na kipo katika hali nzuri ya kutoa huduma hivyo wapo tayari kutoa huduma.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam Sporah Liana amesema ifikapo siku ya Jumanne watafanya kikao na Wafanyabiashara wote watakaokuwa wakitoa huduma ndani ya jengo na siku ya Jumatano watakutana na Wamachinga, Baba lishe na Mama lishe kwa ajili ya kuwekeana mikakati ya biashara.

Naye Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam Lazaro Mambosasa amesema Jeshi la Polisi limejipanga kuhakikisha abiria wote wanaosafiri au kuingia kituoni hapo hawapati usumbufu wa aina yoyote.