
Ansu Fati akishika goti lake baada ya kupata maumivu mwaka jana novemba 7.
Ansu Fati alipata majeraha ya goti tarehe 7 Novemba mwaka 2020 wakati klabu yake ya Barcelona ilipokuwa inacheza na Real Betis, baada ya majeraha hayo Fati alifanyiwa upasuaji wa goti lake la kushoto tarehe 9 Novemba mwaka jana na kutathminiwa kurejea Machi 10 mwaka huu.
Taarifa kutoka klabu ya Barcelona zinaeleza kuwa wakati Ansu Fati anakaribia kurejea dimbani hivi karibuni, amepatwa na majeraha mengine kwenye goti hilo hivyo atalazimika kufanyiwa upasuaji mwingine ambao bado haujajulikana utamuweka nje kwa muda gani.
Kutokana na kuwa nje ya uwanja kwa miezi minne iliyopita baada ya upasuaji wa awali, hofu imekuwa kubwa kwamba huenda baada ya upasuaji wa awamu hii ya pili ukatazamiwa kumuweka nje zaidi ya miezi miwili hadi mitatu na kumfanya kukosa michezo yote ya msimu huu na EURO Juni 11, 2021.
Kwa upande wa Ansu Fati mwenyewe, siku mbili zilizopita alisema “Nina imani nitakuwepo kwenye EURO 2021, lakini ninahitaji kupona kikamilifu. Sijui nini kitatokea siku za usoni, lakini ni ndoto yamchezaji yeyote kucheza michuano hiyo.”
Fati mwenye umri wa miaka 18, amecheza michezo 10 pekee kwenye michuano yote msimu huu, 7 ya ligi kuu Hispania na 3 ya ligi ya mabingwa barani Ulaya na kufunga mabao 5 huku akitengeneza mabao 2.
Kama atafanikiwa kupona mapema, Ansu Fati ataiwakilisha nchi ya Hispania kwa mara ya kwanza kwenye michuano rasmi mikubwa ukiondoa michezo ya kuwania kufuzu michuano hiyo.