Monday , 26th Apr , 2021

Mshambuliaji wa zamani wa Newcastle United Alan Shearer na mshambuliaji wa zamani wa Arsenal Thierry Henry wamekuwa wachezaji wawili wa kwanza kutunukiwa tuzo ya heshima ya juu ya soka kwenye Ligi Kuu nchini England (Hall of Fame).

Thierry Henry (kushoto) Alan Shearer (kulia)

Shearer ndiye mfungaji bora wa muda wote wa Ligi Kuu England, akiwa amepachika mabao 260 katika misimu 14 ya Ligi hiyo akiwa na vilabu vya Newcastle united na Blackburn Rovers.

Mchezaji huyo wa zamani wa kimataifa wa England, ambaye alishinda taji la Ligi Kuu msimu wa 1994-95 na Blackburn, ndiye mchezaji pekee aliyefunga mabao 100 ya EPL akiwa na timu mbili tofauti.

Tuzo hiyo pia ilikabidhiwa kwa mchezaji wa zamani wa Ufaransa Thiery Henry aliyeifungia klabu ya Arsenal jumla ya mabao 175 kwenye kwenye Ligi hiyo katika mechi 258 na alikuwa sehemu ya kikosi cha The Gunners kilichoshinda Ubingwa wa EPL msimu wa 2001-02 na ule wa msimu wa 2003-04 ambao walishinda bila kupoteza mchezo hata mmoja.

Taarifa iliyotolewa na Ligi hiyo imesema tuzo hiyo ya heshima ni sehemu ya kutambua mafanikio na vipaji vya wachezaji walishiriki katika ligi hiyo kuanzia mwaka 1992, na wachezaji wanao shinda tuzo hii ni wale waliostaafu kuanzia Agosti 1, 2020.