Thursday , 29th Apr , 2021

Mwanadiplomasia na mchambuzi wa masuala ya siasa Goodluck Ng'ingo, amesema kuwa Rais Samia Suluhu Hassan akishika nafasi ya Uenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), na kuzisimamia kanuni za maadili ya uongozi basi ile presha ya wanachama nje ya mfumo rasmi haitaonekana.

Kushoto ni Mwanadiplomasia na mchambuzi wa masuala ya siasa Goodluck Ng'ingo na kulia ni Rais Samia Suluhu Hassan

Ng'ingo ametoa kauli hiyo hii leo Aprili 29, 2021, kwenye kipindi cha SupaBreakfast cha East Africa Radio na kuongeza kuwa endapo atalegea kuzisimamia kanuni hizo basi kila mtu atapata mwanya wa kutoa dukuduku lake hususani wale wenye makundi yanayowahitaji watu fulani kwenye uongozi kwa sababu zao binafsi.

"Ukitazama Chama cha Mapinduzi (CCM), kina kanuni za maadili ya uongozi ambayo kwenye zile kanuni zimeeleza taratibu na miiko ya mwanachama na vilevile kinaeleza kuwa moja wapo ya makosa ambayo yanaweza kuhesabika kama usaliti ni kupinga maamuzi ambayo yanatokana na vikao halali vya chama", amesema Ng'ingo.

Aidha ameongeza kuwa "Ni kwa namna gani Rais Samia ataweza kusimamia kanuni za maadili za uchaguzi na viongozi wa chama ni jambo lingine, kama atazisimamia tunategemea lile joto tunaloliona nje ya mfumo rasmi wa chama hatutaliona, maana yake watendelea kuparuana ndani ya chama".