
Mchungaji Merchades Mugishagwe na mkewe Agripina Maganja
Mchungaji Merchades Buberwa Mugishagwe na mke wake Agripina Maganja walifikishwa katika Mahakama hiyo Februari mwaka huu wakikabiliwa na mashtaka manane likiwamo la kushindwa kutimiza wajibu wao kama wazazi wa kuwapeleka watoto wao watatu shule, wakidai kuwa kufanya hivyo ni dhambi, maana maandiko ya Mungu hayaruhusu watoto kwenda shule.
Akizungumza mahakamani hapo wakili wa serikali Grey Uhagile, amesema kuwa walikuwa wakisikiliza upande wa utetezi ambao mpaka sasa wamemaliza kujitetea na sasa wanasubiri maamuzi yanayotarajiwa kutolewa Agosti 16 mwaka huu.
Kwa upande wake wakili wa utetezi Rogate Assey, amesema kuwa ushahidi wa kesi hiyo umefungwa na kwamba wameshindwa kumpata shahidi wa tatu ambaye ni Mungu anayetajwa na washtakiwa hao.
Wakili Assey amesema kuwa mashahidi wote walikuwa wakisema aliyezuia watoto wasiende shule ni Mungu na maandiko yanakataza elimu ya dunia, kwa hiyo kwa mujibu wa sheria ingewezekana Mungu aitwe mahakamani atoe ushahidi kwamba ni kweli aliwazuia labda angeitwa, lakini kwa sababu hata wangesema aitwe hawawezi kumtumia wito, kwahiyo imeshindikana na wamefungia ushahidi wao hapo.
Watoto hao mkubwa wa kike akiwa na umri wa miaka 13, wa pili wa kiume miaka tisa na wa tatu wa kike miaka mitano, Februari mwaka huu walipelekwa shule kwa lazima na serikali na sasa wanaendelea na masomo katika shule ya msingi Mugeza Mseto iliyoko katika Manispaa ya Bukoba.