Wednesday , 22nd Sep , 2021

Makala ya kutangaza vivutio vya utalii, biashara na uwekezaji iliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan, ambayo itaoneshwa kwenye kipindi maarufu cha Royal Tour, zimeanza kuzaa matunda baada ya wawekezaji kujitokeza kwa uwekezaji wa hoteli za kisasa ndani ya Hifadhi za Taifa.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hasaan

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Damas Ndumbaro, mara baada ya mkutano  wake maalum na wawekezaji kutoka nchi ya Bulgaria uliofanyika jijini Dar es Salaam, ambapo wameahidi kujenga hoteli zenye hadhi ya nyota tano kwenye hifadhi 4 za Taifa ambazo ni Kempinski Serengeti,  Kempinski Manyara, Kempinski Tarangile na Kempinski Ngorongoro.

''Juhudi kubwa za kimkakati za Royal Tour zilizoendeshwa na Rais wetu zimeweza kuzaa matunda ambapo leo tumepokea wawekezaji mahiri kutoka Bara la Ulaya ambao watawekeza kwenye hoteli kwa kujenga hoteli tatu za nyota tano za 'brand'  ya  Kempinski  kwa uwekezaji wa Dola za Kimarekani Milioni 72," amesema Dkt Ndumbaro

Waziri Dkt. Ndumbaro ameongeza kuwa,  ujenzi huo ni mkubwa na unakadiriwa kuanza rasmi mwezi Januari 2022 ambapo amemshukuru Rais Samia kwa kuwezesha kuwapigia 'pass' na wao kupitia Wizara ya Maliasili ni utekelezaji ikiwemo kupokea wawekezaji.