
(Kocha wa Yanga, Mohammed Nasreddine Nabi na kocha wa Namungo,Hemed Selemani 'Morocco')
Morocco amesema, "Yanga imeanza vizuri na kuonekana bora, Ukiangalia kiufundi hawajakamilika kwa asilimia zote. Wanaupungufu ambayo tutautumia kutafuta matokeo chanya ili kuondoka na pointi tatu katika mchezo huo"
"Hatuwezi kuweka silaha zetu kwa wapinzani wetu, ila tunaingia kwa staili nyingine na mbinu tofauti tofauti na mechi tano tulizocheza."
"Tumejiriimarisha kila idara na hatutowapa nafasi washambuliaji wa wapinzani kuleta madhara ili kuhakikisha tunapata pointi tatu katika mchezo huo na kujiweka sehemu salama katika msimamo" Amesema Morocco.
Kwa upande wa kocha wa Yanga, Mohammed Nasreddine Nabi amesema wanaendelea kufanyia kazi mapungufu yao na ubora wa Namungo ili kuhakikisha wanaendelea kufanya vizuri.
Nabi amesema, "Tulikuwa na wakati mzuri Zanzibar, tumepata nafasi ya kupanga mambo yetu licha ya ushindi tuliopata visiwani humo katika michezo yetu miwili lakini kuna mambo mengi tumeweza kuyaboresha pamoja na kuwa na wachezaji wachache"
"Hatuna mechi iliyokuwa rahisi kwetu, tumewaona Namungo FC wanavyocheza tumeanza kufanyia kazi mapungufu yetu na ubora wa Namungo FC kuhakikisha tunaendelea kupata matokeo chanya na kufikia malengo yanayotarajiwa ya kuteaa ubingwa". Amegusia Nabi.
Namungo ipo nafasi ya 11, baada ya kucheza michezo 5 nakukusanya alama 5 wakati Yanga ni kinara akiwa na ushindi wa asilimia 100 baada ya kushinda michezo yake yote mitano na kuwa na alama 15.
Rekodi zinaonesha kuwa, tokea Namungo ipande Ligi Kuu msimu wa mwaka 2019-2020 imecheza michezo 5, Yanga ikishinda mmoja pekee Januari 8, 2021 kwa bao 1-0 la Zawadi Mauya huku wakitoka sare mara 4.