Wednesday , 8th Dec , 2021

Zikiwa zimesalia siku tatu kuelekea kwenye mchezo wa Kariakoo Derby, Simba na Yanga Disemba 11, 2021 kwenye dimba la Mkapa, Maaofisa habari wa vilabu hivyo wametambiana kuondoka na alama tatu muhimu.

(Hassan Bumbuli wa Yanga (kushoto) na Ally Shatry wa Simba (kulia))

Kaimu Ofisa Habari wa Simba, Ally Shatry amesema, Simba haifungwi mara mbili na Yanga wakati Hassani Bumbuli amesema kwa maandalizi  waliyofanya basi wataondoka na alama tatu na kushangilia kama mshmabuliaji wao Fiston Mayele.

Ally Shatry almaarufu ‘Chico’ amesema: "Tunajua Yanga ilitufunga katika mchezo wa Ngao ya Jamii lakini siku zote Simba haifungwi mara mbili. Jumamosi ni zamu yetu maandalizi ya mchezo yanaendelea vizuri. Timu imeingia kambini jana baada ya kurudi kutoka Zambia na wachezaji wote wapo kwenye hali nzuri”.

Kwa upande wa Yanga, Hassan Bumbuli amesema: "Staili yetu ya kushangilia ni ile ile maarufu nchini ya Fiston Mayele, kitu kizuri kinaigwa hata watani mkitaka sio mbaya kuiga. Maandalizi yamekamilika tutamkosa Yacouba Sogne pekee ambaye ni majeruhi wengine wote wapo fiti tayari kwa mchezo. Kwa maandalizi tuliyofanya tunaamini tutaibuka na ushindi”.

Mchezo huo unataraji kuchezwa saa 11:00 Jioni Disemba 11, 2021 Jumamosi kwenye dimba la Benjamin Mkapa huku Simba ikiwa na kumbukumbu ya kufungwa 1-0 kwenye fainali ya ngao ya Hisani disemba 25, 2021.