Monday , 17th Jan , 2022

Shahidi wa pili wa utetezi katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Lengai Ole Sabaya na wenzake, Jesca Thomas ameieleza mahakama kuwa akiwa hotelini Dar es Salaam na aliyekuwa DC Hai, ambaye ni mchumba wake walivamiwa na kukamatwa na polisi waliokuwa wamevalia nguo za kiraia na silaha.

Jesca Thomas (Mchumba wa Sabaya), na kulia ni aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya

Januari 14, 2022, Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha iliwakuta na kesi ya kujibu watuhumiwa saba, akiwemo Sabaya mwenyewe, katika kesi ya uhujumu uchumi namba 27 inayowakabili, na leo utetezi umeanza.

Lengai ole Sabaya pamoja na wenzake 6 kwenye kesi hiyo ya uhujumu uchumi wanakabiliwa na tuhuma za kuchukua kiasi cha shilingi milioni 90 kutoka kwa mfanyabiashara Francis Mrosso kwa madai kwamba amekwepa kodi.

Shahidi wa kwanza wa utetezi Silivester Nyegu, ambaye pia ni mshtakiwa katika kesi hiyo amekana shtaka hilo na kuieleza mahakama kuwa hakuwahi kushiriki na wala kupata mgao wa pesa hizo na hakuwahi kujihusisha katika genge la uhalifu.