Monday , 31st Jan , 2022

Michezo ya mtoano hatua ya 32 bora ya Kombe la TFF ASFC 2021-2022 imehitimishwa jioni ya jana Januari 29, 2022 kwa michezo mitatu iliyochezwa kwenye viwanja mbali mbali.

(Matukio mbalimbali ya vigogo katika hatua ya 32 bora ya TFF ASFC 2021-22)

Walima Miwa kutoka mkoani Morogoro, Timu ya Mtibwa Sugar iliifunga African Sports ya ‘Championship’ kwa penalty 4-2 baada ya sare ya bili kufungana katika dimba la Mkwakwani Jijini Tanga.

Kagera Sugar ‘Wanankurukumbi’ wameendelea kupata matokeo mazuri baada ya kuifunga timu ya African Lyon ya ‘First Division’ mabao 4-0 huku kiungo wake mshambuliaji, Meshack Abraham akifunga ‘Hat Trick’ kwenye dimba la Chamazi.

Bingwa mtetezi wa kombe hilo, Mnyama Simba SC, iliiangushia kapu la magoli timu ya Dar City ya ‘First Division’ kwa kuifunga mabao 6-0 bila huruma baada ya kucheza michezo mitatu kufungwa miwili na sare ya bila kufungana.

Mabao ya Simba SC yamefungwa na Meddie Kagere aliyefunga mabao mawili, Clatous Chama aliyekuwa kwenye kiwango bora kwa kufunga na kutengeneza mabao mawili, Larry Bwalya, Pascal Serge Wawa na Chris Mugalu akifunga la sita.

 Kwa matokeo hayo, droo ya TFF ASFC imeshapangwa na kuwekwa hadharani na kuonesha kama ifuatavyo:

Bingwa mtetezi Simba SC itacheza na Ruvu Shooting, Yanga SC itakipiga na Biashara United, Pamba dhidi ya Dodoma Jiji, Tanzania Prisons dhidi ya Polisi Tanzania, Coastal Union na Mtibwa Sugar wakati Kagera Sugar na Namungo FC. 

Baga Friends watacheza na Bingwa wa Kombe hilo wa mwaka 2019, Azam FC wakati mchezo ulio hairishwa kati ya Mbuni FC na Lipuli FC mshindi wa mchezo huo atacheza na Geita Gold FC.

Michezo ya hatua Robo fainali itapangiwa tarehe kuanzia mwezi ujao.