Tuesday , 10th May , 2022

Umoja wa Ulaya (EU) nchini Tanzania umekutana na kusherekea kwa pamoja "Siku ya Umoja wa Ulaya" baada ya kupita miaka miwili pasipokufanyika sherehe hizo nchini hapa.

Balozi Manfredo Fanti, Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania

Sherehe hizo zimekuwa zikifanyika nchini lakini kwa mwaka 2020 na 2021 sherehe hizo hazikufanyika, sherehe za "Siku ya Umoja wa Ulaya" huwaleta pamoja nchi wanachama wa umoja huo ambao balozi zao zipo Tanzania ili kusherekea mafanikio ya ushirikiano wa Tanzania na nchi hizo.

Akizungumza katika sherehe hiyo Jijini Dar es salaam, Balozi wa EU nchini Tanzania Balozi Manfredo Fanti amesema wazi kwamba wanajivunia ushirikiano na Tanzania na kwamba wamekuwa msitari wa mbele katika kukuza maendeleo ya Watanzania kupitia kilimo na sekta nyingine mhimu.

"Tunaposherekea siku hii tunafurahia ushirika wetu na Tanzania, tumekuwa na uhusiano wa karne na Tanzania na tumekuwa tukichamgia katika maendeleo ya Watanzania. Tumekuwa tukitoa misaada ya kila aina kuinua sekta ya kilimo na biashara ili kuwapatia watu kipato na kuleta maendeleo nchini, lakini tumejidhatiti kuhakikisha kwamba tunaendelea kufadhili mikakati mbalimbali ili Tanzania iwe na mendeleo na mafanikio kwa watu wa Tanzania" - Manfredo Fanti, Balozi wa EU Tanzania.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Balozi Liberata Mulamula ambaye ndiye mgeni rasmi katika sherehe hiyo, amesema Tanzania inajivunia ushirika wake na EU na kwamba imekuwa ikipata fedha nyingi kutoka EU suala ambalo limekuwa likiharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini.

"Kwakweli EU wamekuwa wadau wetu wa muda mrefu, na wao wakitoa pesa wanatoa pesa nyingi sana na kuturahisishia sisi kutekeleza miradi yetu kwa wakati. Lakini pia tu ajivuania ushirikiano huu kwasababu kwa mfano hivi karibuni Mhe. Rais amefanya ziara huko na tumegundua wanauhitaji wa mchele, tuna mashamba kwahiyo Watanzania tutumie hii fursa ya kilimo - biashara tupate pesa" - Balozi Liberata Mulamula, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania.

Aidha, katika sherehe hiyo miongoni mwa waliohudhuria ni aliyekuwa waziri wa mambo ya nje wa Tanzania Profesa Palamagamba Kabudi ambaye ameiambia EATV kwamba EU wamekuwa wadau wakubwa wa maendeleo ya Tanzania kwa muda mrefu na kuwa ni wakati wa kushirikiana zaidi kwenye uwekezaji na biashara kuliko misaada.